11 March 2013

Manyanyaso ya wanawake duniani yakomeshwe



PAMOJA na umri mkubwa tangu kuanza kwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, bado tunachoshuhudia katika jamii zetu ni manyanyaso mbalimbali wanayofanyiwa akina mama duniani.


Hali za kuwatumia kinamama katika mazingira ya kivita inasikitisha kwani takwimu zinaonesha wazi kuwa bado kuna idadi kubwa sana ya kinamama na hasa walio katika umri wa ujana wanaendelea kunyimwa haki zao katika mazingira mbalimbali yanayotawaliwa na vita na vurugu.

Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa ni tabaka linalodai haki dhidi ya mfumo dume, haki ya usawa kijinsia katika elimu, kazi za kiuchumi na kijamii.

Haishangazi kuona kuwa wanawake wamekuwa na vyombo vingi vinavyowatetea, zikiwemo asasi za kiraia na za kiserikali na mashirika ya sheria, lakini tatizo limekuwa ni kubwa kwao.

Tangu shuleni wanawake wanapewa upendeleo, ukifika bungeni kuna viti maalumu vya wanawake, hiyo yote ni njia ya kuwawezesha wanawake. Lakini kwa nini wanawake wanatetewa kiasi hicho?

Je, ni kweli wanawake hawawezi? Mimi nadhani sasa ifike mahali wanawake wajitokeze wapaze sauti yao wenyewe badala ya kusubiri kuwezeshwa.

Nasema hivi kwa sababu wanawake ni binadamu yule yule kwa hiyo, hana tofauti na mwanaume kiutendaji ukiacha tofauti ya jinsia tu. Mwanamke anaweza kufanya kazi zote zinazofanywa na wanaume bila kupendelewa, sasa kwa nini asubiri kuwezeshwa?

Tumeona wanawake wakiendesha hata magari ya mizigo, ndege, meli na treni. Siku hizi tunaona wanawake wakicheza hata mpira wa miguu. Hii inaonyesha kuwa wanawake wanaweza kila kazi. Kuendeleza upendeleo ni hali ya kuonyesha kwamba hawawezi na hii inawaathiri kisaikolojia.

Kwa upande mwingine, hapa Tanzania, ukombozi wa mwanamke unakwamishwa na wanawake wenyewe. Kuna haja ya wanawake Tanzania kujifunza kutoka mataifa mengine. Sherehe kama hii ya siku mwanamke duniani iwe ni fursa ya kujifunza kutoka kwingine.

Tanzania ni lazima tupige hatua katika jitihada za kumkomboa mwanamke. Kuna kazi kubwa ya kuvunjilia mbali mfumo dume ambao kwa kiasi kikubwa umejengeka kiasi hata wanawake wanafikiri na kutenda “kimfumo dume”.

Akigombea mwanamke, wanawake wenzake wanakuwa mstari wa mbele kusema kwamba hawezi na wakati ukifika wa kupiga kura wanamnyima kura zao. Ipo mifano mingi ya wanawake kushindwa kuwaunga mkono wanawake wenzao na kuwapigia kura wanaume. Hali hii ni hatari.

Hivyo wanawake pia ninashauri wanawake tuwe mstari wa mbele kupendana tuache mfumo dume ambao sasa tunaupandikiza sisi wenyewe.Mwisho ninawatakiwa sikukuu njema.

No comments:

Post a Comment